Wavuvi wa eneo la Mji wa kale mjini Mombasa wanaitaka Serikali ya kaunti hiyo kulifungua soko la samaki ambalo limesalia bila kutoa huduma kwa wavuvi hao kwa muda mrefu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na Mwenyekiti wa wavuvi wa eneo hilo la Kibokoni Abdulghan Golloh, licha ya wavuvi hao kuwasilisha lalama zao kwa Gavana wa kaunti hiyo Ali Hassan Joho na kuahidi kulifungua lakini bado halijafunguliwa.

Wavuvi hao sasa wanalazimika kuuza samaki wao nje ya soko hilo huku wengine wakiuza samaki katika fuo za Bahari hindi.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumamos , Golloh amesema kuwa soko hilo kwa sasa liko katika hali duni, na licha ya Rais Uhuru Kenyatta kuzuru soko hilo, hakuna hatua zozote mwafaka zilizochukuliwa.

"Tunashangazwa na uongozi wa Gavana Joho kwa kutuahidi kuimarisha soko la samaki ili tufanye biashara, lakini mpaka sasa bado, sasa sisi hatuna mahali maalum pa kuweka biashara zetu, tunaomba serikali kuu iingile kati swala hili na kutusaidia nasi tujikimu kimaisha," alisema Golloh.

Golloh amedokeza kuwa hatua ya wachuuzi hao kufanya biashara zao nje ya soko hilo kamwe haifai, na ni vyema iwapo serikali kuu na ile ya kaunti ya Mombasa zitashirikiana kutatua shida hiyo.

Picha: Wavuvi Mombasa wakizungumza na wanahabari jinsi biashara yao ya kuuza na kuvua samaki bado haijaangaziwa vyema na serikali kuu na ile ya kaunti ya Mombasa.