Viongozi wa Kanisa la kiadventista katika eneo la Nyanza wamewataka viongozi wa kisiasa kutoka eneo hilo kuzingatia na kutilia maanani maendeleo ya raia na kukoma kulumbana kila wanapokutana kwenye maeneo ya siasa.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakihutubu kwenye mazishi ya muumini wao katika eneo la Katito, Kaunti ya Kisumu mnamo siku ya Jumanne, viongozi hao walishtumu mizozo ya chini kwa chini inayoendelea kwenye Bunge la Kaunti ya Kusumu, ambapo wawakilishi wa Wadi wanatofautiana kila mara wakati wanapopitisha miswada bungeni.

“Tumechoka kuona vioja kwenye Bunge la Kaunti ya Kisumu na tunawataka viongozi wetu walio kwenye Kaunti ya Kisumu kuzingatia na kutilia maanani maendeleo ya nchi na kutupilia mbali tofauti zao za kisiasa,” alisema Kasisi Linus Abondo.

Mwenyekiti wa makasisi hao, Tomothy Onyonga alionya kwamba hali hiyo inanuia kusambaratisha maendeleo ya kaunti na hivyo basi ni sharti ikomeshwe kwa kaunti hiyo kuona maendeleo dhabiti yanayotokana na ugatuzi kwenye siku za usoni.

“Ugatuzi ni chombo cha maendeleo dhabiti na viongozi wetu hawanabudi kuheshimu utawala wa kaunti kwa kuwaletea wananchi maendeleo mashinani kuliko kushinda wakilumbana kwa tofauti zao za kisiasa,” alisema Onyonga.

Aidha, viongozi hao kwa kauli moja waliwataka wawakilishi hao pamoja na viongozi wengine waliochaguliwa na wananchi kuhakikisha kwamba wanatimiza ahadi walizotoa kwenye sera zao wakati wa kampeni kabla ya kuchaguliwa kwenye uchaguzi mku wa mwaka 2013.