Kulikuwa na vurugu katika bunge la Kaunti ya Mombasa pale wawakilishi wa wadi walipozozana baada ya kutofautiana kuhusu suala la kumuondoa mamlakani spika wa bunge hilo Thudius Rajwayi.
Purukushani hiyo ilianza pale spika alipowaamuru wawakilishi wadi wawili kuondoka bungeni kufuatia utovu wa nidhamu baada ya kutofautiana kuhusu swala hilo la kumuondoa Rajwayi.
Bunge hilo la kaunti lilikuwa limegawanywa katika makundi mawili, moja likiunga mkono spika huyo huku hilo lingine likimpinga.
Kundi moja lilikuwa likiongozwa na mwakilishi wa Wadi ya Kongowea Jabez Oduor huku hilo lingine likiongozwa na mwakilishi wadi mteule Mohamed Khatimy.
Hatimy alianza kupigana na Oduor aliyekuwa amekaa kando yake, hatua iliyomlazimu spika kuwaamuru kuondoka bungeni.
Wawakilishi wadi waliokuwa wakitaka spika huyo kutimuliwa walikasirishwa na hatua hiyo huku wakianza kuwarushia wenzao makonde.
Wawakilishi wadi waliomtaka Rajwayi ang'atuke mamlakani waling’oa picha zake kutoka kutani.
Inadaiwa kuwa ofisi za spika, kiongozi wa walio wengi pamoja na kiongozi wa wachache zilifungwa na watu wasiojulikana wakati bunge hilo lilikuwa kwenye likizo.
Bungeni hilo lilikuwa linarejelea vikao vyako baada ya kuwa katika likizo ya muda.