Wawakilishi wa wadi katika kaunti ya Nyamira wamekataa ripoti ya kamati iliyoundwa kuwachunguza maafisa waliohusishwa na sakata ya ufisadi.
Ripoti hiyo ambayo ilifikishwa katika bunge la kaunti hiyo siku ya Jumatatu kupitia mwenyekiti wa kamati hiyo James Isabwengi inasema kati ya maafisa sita waliosimamishwa kazi kwa madai ya ufisadi ni maafisa wawili pekee waliojihisisha na ufisadi na kuomba wengine wanne kuondolewa madai hayo.
Wawakilishi hao wa wadi wakiwa chini ya uongozi wa spika wa kaunti hiyo Joash Nyamoko waliikataa ripoti hiyo na kusema ni ya uongo huku wengi wakisema kuwa maafisa wote sita walijuhusisha na ufisadi.
“Ripoti hiyo itarejelewa mara ya pili baada ya uchunguzi mwingine mpya kufanywa ili kuzungumziwa mara ya pili bungeni,” alisema Nyamoko.
Baadhi ya maafisa waliohusishwa kwa ufisadi ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Fedha John Omanwa na Mkuu wa Idara ya Michezo na Utamaduni Peter Omwanza.
Maafisa walioondolewa madai ya kujihusisha na sakata hiyo ya ufisadi kulingana na ripoti hiyo ni Mkuu wa Idara ya Maji Andrew Ombati, Mkuu wa Idara ya Barabara Kepha Osoro, Fridah Nyaboga na Morara Mokua.
Kamati iliyoundwa kufanya uchunguzi huo ilitembelea miradi mbalimbali iliyofanywa na maafisa hao walipokuwa mamlakani ili kufanya uchunguzi wao.