Shirika la 'Centre for Enhancing Democracy and Good Governance' (CEDGG) sasa linataka serikali ya Kaunti ya Nakuru kuweka bayana lengo la ziara iliyofanywa hivi maajuzi wa mawaziri na wawakilishi wa kaunti ya Nakuru mjini Mombasa.
Akizungumza katika mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Nairobi, afisa anayesimamia miradi katika shirika hilo Masese Kemunche alisema kwamba lengo haswaa la ziara hiyo iliyofanywa takriban wiki mbili zilizopita halikuwekwa wazi.
“Swala hili la serikali ya Kaunti ya Nakuru kwenda Mombasa kwa wiki moja ni swala ambalo liliweza kutupelekea kuibua maswali kama shirika. Madhumuni ya kwenda Mombasa hayakubainika. Wanapokariri kuwa walienda Mombasa kuendeleza shughuli za kuwaleta pamoja kama kundi, matamshi haya yanaashiria kwamba kunaweza kuwa na tatizo,” alisema Kemunche.
kulingana na Kemunche, safari hiyo ilitokea wakati mkaguzi wa fedha za umma alipotoa ripoti kuhusu matumizi ya pesa za umma kwenye kaunti, jambo ambalo anadai lilionyesha kuwa safari ya viongozi hao wa kaunti ilinuiwa kuficha matumizi yasiyofaa ya fedha hizo.
Hata hivyo, Peter Mbae, ambaye ni mwanachama wa bodi ya utumishi wa umma katika kaunti ya Nakuru aliwarai wanahabari kupata habari kamili kabla ya kuripoti taarifa za kaunti.
Alikosoa ripoti zilizochapishwa kwa vyombo vya habari kuhusiana na ziara hiyo ya wawakilishi wa wadi mjini Mombasa, iliyodaiwa kugharimu kaunti mamilioni ya pesa.