Baadhi ya wawakilishi wa wadi katika bunge la kaunti ya Nakuru wameizomea serikali ya Nakuru baada ya kuibuka madai kwamba vibarua wengi hasua kutoka mjini Naivasha hawajalipwa mishahara yao kwa muda wa miezi sita.
Wawakilishi wadi hao sasa wanataka pesa ambazo zimo kwenye akaunti ya serikali hiyo na ambazo hazijatumiwa zitumiwe kuwalipwa wafanyakazi hao.
Mwenyekiti wa kamati ya utekelezaji katika bunge hilo Simon Wanyoike Wanango alisema kuwa fedha zilizotengewa kupanuliwa kwa barabara moja karibu na bunge hilo pia, zinafaa kutumiwa kuwa minajili ya kuwalipa wafanyakazi hao.
“Tulikuwa tumetenga shilingi milioni sitini kwa upanuzi wa barabara hiyo. Kwa sababu hazikutumika, sasa zielekezwe kuwalipa wafanyakazi hawa. Pia wana familia ambazo zinahitaji maisha bora kama wengine,” alisema Wanango.
Kwa mujibu wake, mradi wa upanuzi wa barabara hiyo haukuendelea baada ya kuibuka kuwa haimo chini ya mamlaka ya ujenzi wa barabara za kitaifa KeNHA.