Wawakilishi katika bunge la Kaunti ya Mombasa wamemlaumu mshirikishi wa usalama katika kanda ya Pwani Nelson Marwa, kwa madai ya kuamrisha ubomozi wa nyumba zilizoko karibu na Uwanja wa Ndege wa Moi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakizungumza katika bunge hilo siku ya Jumanne, wawakilishi wadi hao walidai kuwa Marwa amekuwa akiingilia maswala yanayohusu uongozi wa kaunti hiyo bila kutafuta ushauri.

Aidha, walidai kwamba Marwa alimuandikia barua mwenyekiti wa Tume ya Ardhi nchini Mohamed Swazuri, kuelezea jinsi wakaazi wanaoishi karibu na uwanja huo wa ndege watakavyoondolewa na nyumba zao kubomolewa.

Mbali na nyumba za makaazi kubomolewa, inadaiwa kuwa shule pamoja na majengo ya biashara katika eneo hilo zitabomolewa kutokana na sababu za kiusalama.

Hata hivyo, wawakilishi hao walimlaumu mshirikishi huyo kwa kile walichokitaja kama kuingilia majukumu ya kaunti wakiongeza kuwa mageuzi kama hayo hutekelezwa na wizara husika katika kaunti.

“Tuna kiongozi anayeshikilia Kaunti ya Mombasa na si mwingine bali ni Hassa Joho. Kwa hivyo, kama Marwa amezunguka akashindwa, aache kuingilia mambo ya ardhi,” alisema Ibrahim Abdallah, mwakilishi wa Wadi ya Kipevu.

Viongozi hao wametoa wito kwa wananchi wanoishi eneo hilo kususia mpango wa kuondolewa hadi pale swala hilo litakapowekwa wazi.