Kufuatia kuongezeka kwa visa vya utovu wa usalama katika maeneo mengi kaunti ya Nyamira, sasa wawakilishi wadi wa bunge la kaunti hiyo waitaka serikali ya kitaifa kumhamisha kamishna wa kaunti hiyo Josphine Onunga.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakihutubu walipoitembelea familia ya wahasiriwa wa tukio la mauaji ya Kinyama kule Nyamusi siku ya Jumatano, wawakilishi hao walimpa kamishna wa kaunti hiyo ilani ya mwezi mmoja kurekebisha hali au kuondoka katika kaunti hiyo.

"Haiwezekani kwamba kila mara wananchi wanavamiwa na majambazi na kisha kuporwa mali yao ilhali tuna idara inayostahili kuwahakikishia usalama wao, na ndio maana twampa ilani kamishna Onunga kurekebisha hali au aondoke," alisema Kiongozi wa wengi Laban Masira. 

Masira aidha aliitaka serikali ya kitaifa kuongeza idadi ya maafisa wa polisi wanaofanya oparesheni katika maeneo ya Orwaki, Nyakaranga, Nyamusi, Matongo na Chabera ili kusaidia kuthibiti visa vya uhalifu.

"Nadhani njia ya pekee ya kusaidia kuthibiti visa vya uhalifu humu Nyamira ni kwa kuongeza idadi ya maafisa wa polisi wanaofanya oparesheni katika maeneo ya Orwaki, Nyamusi, Nyakaranga na Chabera," aliongezea Masira.