Wawakilishi wadi kutoka Mombasa wamemtaka Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery, kushughulikia ukosefu wa usalama badala ya kuingilia siasa za kaunti hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kauli hii inajiri baada ya Nkaissery, kumkashifu Gavana wa Mombasa Hassan Joho, kuhusu ufujaji wa fedha za kaunti.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya fedha Mohamed Hatimy, wawakilishi wadi hao walisema Nkaissery amepoteza mwelekeo katika wizara yake, ikizingatiwa hakuna usalama wa kutosha nchini.

“Nkaissery anafaa kuzingatia wizara yake na kuhakikisha kuna usalama wa kutosha badala ya kuingilia siasa,” alisema Hatimy.

Aidha, wawakilishi hao wamemkashifu waziri huyo kwa kukosa kufariji waliopoteza wapendwa wao katika shambulizi la kigaidi huko Mandera, pamoja na wakaazi wa Changamwe waliompoteza afisa wao mkuu wa polisi, na badala yake kuingilia maswala yasiyo muhusu.

Hatimy pia alimkosoa Nkaissery kwa kusema kuwa tangu serikali zigatuliwe, wamepokea shilingi bilioni 13.45 kinyume na shilingi bilioni 32 alizotaja Nkaissery.

Alieleza kuwa katika awamu ya kwanza walipokea shilingi bilioni 3.5, awamu ya pili shilingi bilioni 4.7, na awamu ya tatu shilingi bilioni 5.7.

Hatimy amemtaka Nkaissery kuelezea kwa kina kima cha shilingi bilioni 32 zilikokwenda, iwapo ana uhakika kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa ilipewa pesa hizo.

“Tunamtaka atuelezee kuhusu hizo shilingi bilioni 32 anazosema. Kama zilipewa Kaunti ya Mombasa, atueleze ni lini na wapi,” alisema Hatimy.