Kwa mara nyingine tena wafuasi wa chama cha ODM walimiminika kwenye barabara za mji wa Nyamira kwa maandamano ya kuishinikiza tume ya uchaguzi nchini IEBC kuondoka ofisini.
Wakiongozwa na kiongozi wa walio wengi bungeni katika bunge la kaunti hiyo Laban Masira pamoja na wawakilishi wadi wote wa mrengo wa Cord, waandamanaji hao walisema hawataaacha kuandamana hadi tume hiyo ibanduliwe kwani haiaminiki kuandaa uchaguzi wa mwaka kesho.
"Hatuwezi kuongozwa na wezi kwenye uchaguzi ujao, heri makatibu wa tume hiyo kutuongoza lakini makamishna wote waondoke mara moja," alisema Masira.
Aidha, mweka hazina wa chama hicho katika kaunti ya Nyamira Peter Maroro amesema ni dharau sana kwa wakenya wakati tume hiyo inaendelea kukaa ofisini hata baada ya kuonyeshwa kuwa hawatakikani.
"Isaac Hassan na watu wake waache kutuonyesha madharau sisi ndio wanafanyia kazi na tumewakataa waondoke ofisini mara moja tupate tume mpya," alisema Maroro.
Hata hivyo, maandamano hayo yalisitishwa na maafisa wa polisi ambao waliwazuia waandamanaji hao kuingia katika afisi za tume hiyo IEBC.