Wawakilishi wadi wa kike katika Kaunti ya Nakuru wamelitaka bunge la kitaifa kupitisha mswada wa usawa wa jinsi utakapojadiliwa bungeni tena siku ya Alhamisi.
Wakiongea na wanahabari mjini Nakuru siku ya Jumanne, viongozi hao wakiongozwa na mwakilishi wadi mteule Bi Margaret Wanjiku, walisema kutopitishwa kwa mswada huo hapo awali kulikuwa pigo kubwa kwa utekelezaji wa katiba uliopitishwa mwaka wa 2010.
Bi Wanjiku alisema kuwa kwa mujibu wa katiba, sheria hiyo inafaa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu.
Aliongeza kuwa kutotimiza hayo ni kuweka kazi ya wabunge hao katika hatari.
"Mswada wa usawa wa jinsia haupendelei jinsia moja ama nyingine bali unatoa fursa na nafasi kwa wote katika nyanja tofauti tofauti," alisema Bi Wanjiru.
Aidha, aliwapa changamoto wabunge wanawake kutochoka katika kushinikiza kupitishwa kwa mswada huo.