Kinara wa Cord Raila Odinga amewahakikishia wagombea wote wa nyadhfa mbalimbali kupitia tiketi ya chama cha ODM kwamba kutakuwa na uteuzi wa huru na haki kwenye mchujo.
Raila alipuuzilia mbali madai ya baadhi ya viongozi kuwa watapewa tiketi ya moja kwa moja.
Akiwahutubia viongozi mbalimbali wa ODM pamoja na wananchi huko Ukunda kaunti ya Kwale, baada ya ufunguzi wa afisi za chama hicho, Raila alisema kwamba hakuna mwanachama atakayepewa tiketi ya moja kwa moja.
“Wanachama wote wanaopania kuwania nyadhfa mbalimbali za kisiasa kupitia tiketi za chama hicho sharti wapitie mchujo ulio wa huru, haki na usawa,” alisema Raila.
Matamshi yake yanajiri baada ya kushuhudiwa mgawanyiko kati ya viongozi na wanachama wa ODM katika kaunti ya Kwale, kutokana na madai ya kuwa baadhi ya viongozi huenda wakapewa tiketi ya moja kwa moja kuwania nyadhfa katika uchaguzi mkuu ujao.
Raila aidha ametoa onyo kwa waasi wa chama hicho wanaoshirikiana na mrengo wa Jubilee kuwa watakabiliwa vilivyo na wananchi debeni mwaka ujao.
“Leo hii nataka kuwaambia kuwa safari imeanza bado siku mia tatu na tisini,” alisema Raila.
Wakati huo huo, ameikashifu serikali kwa kusalia kimya na kushindwa kuzuia visa vya mauaji ya kiholela yanayodaiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi.