Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Vijana wawili wenye umri wa makamo wameripotiwa kufariki Jumatano usiku huku mwingine akilazwa hospitalini akiwa na majeraha baada ya kuhusika kwenye ajali iliyofanyika mwendo wa saa kumi usiku katika eneo la Menengai Barabara ya kutoka Mema kwenda Umoja, kaunti ndogo ya Rongai, Nakuru.

Waliofariki ni Tony Ngugu na Njogu Ngugi, huku Martin Kamau akiponea chupuchupu.

Ajali hiyo ilifanyika baada ya marehemu Tony Ngugu aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Mini Canter, kupoteza udhibiti wa gari hilo, na kubingiria mara kadhaa barabarani.

Akidhibitisha ajali hii OCPD wa Rongai Joseph Mwamburi alisema kwamba marehemu wawili hao walifariki wakipokea matibabu kwenye hospitali kuu mjini Nakuru, walikopelekwa baada ya kuokolewa kutoka kwenye mabaki ya gari hilo na polisi.

Miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Nakuru.