Katibu mkuu wa ofisi ya kusajili vyeti vya kuzaliwa katika wilaya ya Kisii ya kati kaunti ya Kisii, Mattews Ayota amewaomba wazazi kuchukua vyeti vyao kutoka ofisi hiyo.
Hii ni baada ya vyeti zaidi ya 3,000 kubaki katika ofisi hiyo kwa muda mrefu bila kuchukuliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa katika ofisi yake iliyoko mjini Kisii, katibu huyo alisema vyeti hivyo vimekuwa kwa ofisini mwake kwa muda mrefu bila kuchukuliwa jambo ambalo limemshangaza sana.
Katibu huyo amewaomba wazazi wote walioenda kwa ofisi hizo na kujaza fomu za vyeti hivyo kuenda kuvichukua na kuviweka mahala pazuri kwani vimekuwa kwa ofisi hiyo kwa muda mrefu sasa.
“Wengi wanakuja na kujaza fomu kwa watoto wao ili wapate vyeti hivyo lakini wakitekeleza shughuli hiyo ya kujaza fomu hawakuji kuchukua vyeti hivyo,” alisema Ayota.
Aliongezea: “Naomba wazazi wale walijaza hizo fomu za kutaka vyeti hivyo vya kuzaliwa kutengenezwa waje ofisini mwangu kuvichukuwa kabla havijaharibika.”
Katibu huyo pia alisema walimu wa shule ndio huwatuma wanafunzi kuwambia wazazi wao waende kujaza fomu hizo.
Alisema kuwa wazazi hao hupanga foleni ndefu na hata kurejea siku ya pili lakini wanapomaliza shughuli ya kujaza fomu hizo hawashughuliki kuchukua vyeti hivyo.
“Naomba wazazi kutupungunzia mzigo wa kuweka vyeti hivyo na waje kuvichukua haraka," alisema Ayota.