Bodi ya kudhibiti pombe kaunti ya Uasin-Gishu imeonya wazazi wenye mazoea ya kupeleka watoto wao katika maeneo kunakouzwa pombe hasa siku za wikendi.
Bodi hiyo inadai kuwa tabia hiyo ndiyo hufanya watoto wengi kuanza kujiingiza katika anasa na uraibu wa dawa za kulevya wakiwa wangali wadogo.
Mwenyekiti wa bodi hiyo Armstrong Rono amesema tabia hiyo ni kinyume cha sheria za watoto hivyo basi wazazi watakaopatikana watachukuliwia hatua za kisheria.
Rono alitaka wazazi ambao hawana shida na watoto wao kunywa pombe wakiwa wangali wadogo kufanyia hivyo katika nyumba zao na wala si katika maeneo ya umma.
“Mzazi yeyote ambaye atapatikana akipeleka watoto mahala ambapo kuna pombe hasa katika baa atatiwa mbaroni,naonya wazazi husika wajihadhari tumeanzisha msako dhidi ya wazazi kama hao,” alisema Rono.
Rono alisema idadi kubwa ya watoto ambao walinaswa wakishiriki anasa katika kilabu moja mjini Eldoret walikiri kuiga tabia hiyo kutoka kwa wazazi na walezi wao.
Wakati huo huo bodi hiyo kwa ushirikiano na vitengo vya usalama ilinasa wanawake kadhaa katika kituo cha kuabiri magari ya uchukuzi wa abiria mjini Eldoret ambao hujifanya wachuuzi ili hali wanauza pombe haramu.
Wanawake hao walinaswa wakiuza chang’a a ambayo ilipakiwa kama maji ya chupa katika kituo kikuu cha kuabiri magari mjini Eldoret.
Rono alifichua kuwa tangu msako dhidi ya pombe haramu uimarishwe wahusika kwa sasa wameanza kutumia mbinu mbadala kuuza pombe hiyo katika maeneo ya umma.
mwisho