Mkuu wa elimu kanda ya Kisumu Mashariki, Bramwel Okoli amewalaumu wazazi ambao hawapeleki wanao shule akisema kwamba idadi ya watoto ambao wanarandaranda mitaani imeongezeka katika maeneo ya Kisumu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kupitia ripoti iliyotolewa na mwalimu mkuu wa wa Shule ya Msingi ya Kachok iliyoko katika Wadi ya Kiboswa Nelson Afubwa, mkuu huyo aliwataka walimu kuwashawishi wazazi katika maeneo hayo ili kuwapeleka shuleni watoto wao ambao wamefikisha na hata kupitisha umri wa kwenda shule.

“Tumepewa ujumbe na Wizara ya Elimu katika eneo hili kwamba tuwahimize wazazi wetu wote kuwapeleka shule watoto wao waliofikisha umri wa kuenda shule. Pia wale ambao wamepitisha umri na hawajawahi kwenda shule waletwe wote,” Afubwa alitoa kauli hiyo shuleni humo wakati wa mkutano na wazazi wa shule hiyo siku ya Ijumaa.

Kwenye ripoti hiyo, mwalimu huyo mkuu alisema kuwa imebainika wazi kwamba baadhi ya wazazi kutoka maeneo hayo wamewatwiga watoto wadogo ambao wanastahili kuwa shuleni majukumu ya kutafutia jamii zao riziki.

“Kwenye pitapita zangu mitaani hapa, hua nakutana na watoto wadogo wakiwa kwenye harakati za kutafuta riziki, ambapo wengine hushinda kwenye masoko wakiuza bidhaa kama njugu karanga na zinginezo huku wengi wakiajiriwa kuchunga mifugo katika maboma ya matajiri,” alihoji mwalimu Afubwa.

Ilibainika wazi kuwa watoto wanao randaranda mjini Kisumu wengi wao wanatoka mitaa ya Mamboleo, Kiboswa, Kowaka miongoni mwa maeneo ya vitongoji duni vingine vya mji huo.

Idadi hiyo ilianza kuongezeka mnamo mwaka 2008 baada ya machafuko yaliyoshuhudiwa nchini baada ya uchaguzi mkuu ambapo familia nyingi zilisambaratika.