Wakazi wa mji wa Molo wamelalamikia ongezeko la bei ya mavazi ya shule, huku shule nyingi zikifunguliwa rasmi kwanzi hii leo, Jumatatu. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza baada ya kununua nguo hizo katika matayarisho ya kufungua shule siku ya Jumapili, Jane Nyokabi, mzazi mmoja katika eneo hilo la Molo alisema bei imepanda kwa kiasi kikubwa. 

"Wamepandisha bei kwa sababu wanajua sharti tuwanunulie wanafunzi sare wanaporudi shuleni," alisema Nyokabi.

Daniel Mogaka, mzazi mwingine alidai kwamba hata viatu vya mitumba ambavyo huuzwa kati ya shilingi mia nne na mia saba vyauzwa kwa bei ya shilingi mia tisa na elfu moja mia tatu. 

"Wauzaji wameamua kututapeli kwa maana hatuna lingine ila kuwatayarisha wanafunzi kurudi shuleni," aliongeza Mogaka.

Mmoja wa wauzaji alisema kwamba hata wao wanauziwa kwa bei kali wanunuapo, na inabidi pia watengeza faida kidogo.

"Katu hatuna haja kuwatapeli wanunuzi wetu, ila maisha ni magumu kwetu pia, tunauziwa bidhaa kwa bei kali," alisema muuzaji huyo.

Shule zinatarajiwa kufunguliwa hii leo, Jumatatu, na imebidi wazazi wafurike mjini kwa matayarisho ya kuwaandaa wanafunzi kurudi shuleni.