Share news tips with us here at Hivisasa

Chama cha wazazi kutoka eneo la Shika Adabu na Likoni, katika Kaunti ya Mombasa, wamezitaka pande zote mbili ya serikali pamoja na upande wa vyama vinavyotetea haki za walimu kunyenyekea ili kupata suluhu la haraka na la kudumu kuhusiana na malipo ya nyongeza ya mishahara ya walimu.

Wakizungumza siku ya Jumapili, wazazi hao walisema kuwa pande hizo hazipaswi kuendelea kuonyeshana ubabe na kuweka siasa huku watoto wakiathirika.

Wakiongozwa na Bi Norah Nyale, ambaye ni katibu wa chama cha SILI, walisema kuwa si haki kamwe kwa mtoto kukaa nje huku serikali ikiendelea kuingiza siasi katika suala hilo.

Wazazi hao waliwataka walimu kuzingatia mwafaka uliotolewa na mahakama kuwa wasitishe mgomo kwa siku tisini na kuandaa mazungumzo katia ya pande zote husika, na kuahidi kuwaunga mkono kupewa nyongeza yao iwapo serikali haitaweka maanani madhila yao.

Nyale alisikitikia hali ambayo inaendelea kukithiri, na kuwashtumu baadhi ya wanasiasa kwa kuendelea kulifanyia suala hilo la mgomo mzaha.

“Badala ya kuendelea kupiga siasa katika maeneo ya hadhara, upande wa upinzani unapaswa kurai serikali kwa njia ya kukubalika kisheria kuwapa walimu mishahara yao na kuleta utatuzi wa kudumu kwa migomo ya walimu ambayo imekuwa ikishuhudiwa tangu nyakati za kupata uhuru,” alisema Nyale.

Alipendekeza kuwe na kikao maalumu baina ya vyama vya kutetea haki za walimu na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, kujadiliana ili watoe maoni yao kwao, badala ya kutoa maoni kwenye vyombo habari, hali ambayo kiongozi huyo alisema imechangia kupanua na kukaza roho za walimu kwa kuhisi kuwa serikali haina nia ya kuwapa haki zao.