Wazazi wa wanafunzi wa shule za chekechea katika kaunti ya Nyamira sasa wamepata nafuu baada ya serikali ya kaunti hiyo kuleta vifaa vya masomo katika shule hizo ambazo wazazi hao wamekuwa wakigharamia. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali hiyo, kupitia Waziri wa elimu Jonnes Omwenga, imepokea vitabu pamoja na vifaa zingine ambazo zimeigharimu serikali hiyo zaidi ya shilingi milioni sita. 

"Tunataka kupunguza gharama ya elimu kwa wanafunzi wa chekechea na pia kurahisishia mzigo wazazi na kwa miaka miwili ijayo elimu kwa shule za chekechea itakuwa ya bure katika kaunti ya Nyamira," alisema Omwenga.

Aidha, serikali hiyo inatarajiwa kuzindua madarasa ambayo imejenga kwa ajili ya wanafunzi hao kote katika kaunti hiyo. 

Mpango huo wa kuinua masomo kwa wenyeji utafaidi wanafunzi zaidi ya 40,000 ambao kwa hivi sasa wamejiunga na shule ya chekechea katika kaunti hiyo. 

"Ni mpango mzuri na kwa hivi sasa tuna zaidi ya wanafunzi elfu arobaini katika shule za chekechea katika kaunti yetu na tunatarajia wengi zaidi kujiandikisha," aliongezea Omwenga.