Serikali ya jimbo la Nakuru kupitia gavana Kinuthia Mbugua imetakiwa kubuni mbinu ya kutoa msaada wa basari mapema, kabla ya shule kufunguliwa ili kuzuia wanafunzi wanaotegemea msaada huo kulipa karo kutotumwa nyumbani au kukosa kufanya mitihani wengine wanapoendelea na masomo.
Wito huu umetolewa na baadhi ya wazazi katika jimbo ndogo la Nakuru kaskazini Jumatatu wikiwakilishwa na Purity Wanjiku na Erastus Maina ambapo wamedokeza kuwa baadhi ya wanafunzi wameanza kutumwa nyumbani baada ya kukosa kulipa karo ya muhula huu.
“Hali ya kutumwa nyumbani kwa wanafunzi kisha kutohudhuria masomo kutokana na ukosefu wa karo, inachangia matokeo duni ya mitihani na ni vyema serikali kubuni mikakati ya kutoa msaada huo kwa wakati unaofaa ili kutotatiza masomo ya wanafunzi,” alisema Wanjiku.
Aidha mwakilishi ya wadi ya Kabazi Mwangi Waithaka amesema ratiba ya kutolewa kwa fedha hizo huzinduliwa na gavana ambako wao husubiri ripoti kutokwa kwa ofisi yake.
“Sisi kama wadau wa hazina za basari huwa tunasubiri hela kutoka kwa ofisi ya gavana kisha baadaye tunasambaza ujumbe kwa umma kuhusu hela zenyewe,” alithibitisha Waithaka.