Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wazazi katika Kaunti ya Nyamira wamehimizwa kuwalinda wanao hasa msimu huu wa likizo ya Desemba ili kuwaepusha watoto hao kutokana na majanga yanayoweza kuwakumba.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatatu, msemaji wa baraza la wazee kutoka Jamii ndogo ya Kiametingi, Nyakwana Orogo, alisema kuwa visa vingi vya ukosefu wa nidhamu huripotiwa hasa msimu huu wa likizo ndefu ya Desemba kwa kuwa wanafunzi wengi huruhusiwa kuhudhuria sherehe mbalimbali bila ya uangalizi wa wazazi.

"Kama wazazi tunajua changamoto zinazowakumba watoto hasa kwenye msimu huu wa likizo ndefu na kwasababu tunajali sana maslahi ya watoto wetu, nawaomba kuchukua jukumu la kuhakikisha kuwa watoto wenu wako salama na kamwe hawajihuzishi na uhalifu wa aina yeyote," alisema Orogo.

Orogo aidha aliwaonya wazazi ambao bado wanaendeleza utamaduni wakuwakeketa watoto wasichana akisema kuwa ukeketaji huo umebainika kuwa na madhara makubwa kwa wanawake.

"Utamaduni wa wazazi kuendelea kuwakeketa watoto wasichana ni utamaduni potovu ambao umepitwa na wakati. Utafiti umeonyesha kuwa ukeketaji wa wasichana huwaathiri pakubwa maishani hasa wanapohitimu umri wakujifungua," alisema Orogo.