Familia moja kutoka kijiji cha Moseri, Kata ya Kiongongi katika Kaunti ya Kisii inatafuta haki ya mtoto wao ambaye aligongwa na gari lililokuwa likienda kwa kasi na kumjeruri mtoto huyo wa miaka mitano alipokuwa akitoka shuleni.
Mzee John Nyasetia na Mama Teresa Moraa ambao ni wazazi wa mtoto huyo wana machungu sana baada ya dereva aliyemgonga mtoto wao kupotea na kukosa kugharamia matibabu ya mwanao ambaye aliumia kwenye kichwa na miguu na kupelekea mtoto huyo kutotembea sawa sawa.
Baba mtoto Nyasetia akiongea na Mwandishi huyu siku ya Jumapili, alisikitikia hali ya mtoto wake ambaye sasa haendi shule kwa sababu ya ajali hiyo ambayo nusura imuue alipokuwa akitoka shule ya Msingi ya Kiongongi.
Nyasetia alisema kuwa msichana wake alikuwa anatoka shuleni tarehe saba mwezi Mei ndiposa akagongwa na gari kwenye ajali. Hata hivyo, Nyasetia alimshukuru Mungu kwa vile gari hilo halikumpotezea maisha ya mtoto wake.
Dereva huyo alipatikana baada ya kijana mmoja wa Bodaboda kumfuata na kumfikia ambapo alimzua na kumlazimisha dereva huyo kumpeleka mtoto huyo hospitalini.
“Dereva huyo aliahidi kushughulikia matibabu ya mtoto wangu hadi apone, lakini hajawahi kurudi tena,” alilalama baba mzazi wa mtoto huyo.
Alisema kuwa mtoto wake bado ana jeraha kwenye kichwa na bado anaendelea kupata matibabu. Pia aliongeza kuwa inawabidi wambebe mwanao kwani hutembea kwa shida kwa sababu aliumizwa vibaya kwenye miguu yake yote.
Ninaiomba Serikali itafute dereva wa gari hilo ambalo lilisababisha ajali hiyo wakisema bado wana nambari za usajili ya gari hilo, ili awalipie bili ya hospitali na afidie mtoto kwani wametumia mali waliokuwa nayo kushughulika matibabu ya mtoto wao na hawana kitu kwa sasa.