Shule ya msingi ya Nyaronge eneo bunge la Bobasi, wadi ya Bassi Masige ambayo vyoo vyake vilijaa itajengewa vyoo vipya hivi karibuni.
Hii ni baada ya mwakilishi wa wadi hiyo Bonface Okenye kuingilia kati.
Akiongea na waandishi wa habari juzi baada ya malalamiko kutoka kwa wazazi na waalimu wa shule hiyo kumfikia Okenye alisema kuwa tayari alikuwa ameongea na mbunge wa Bobasi Stephen Manoti ambaye ameahidi kutenga pesa za maendeleo za maeneo bunge (CDF) kushughulikia swala hilo.
“Nitashughulikia swala hilo haraka iwezekanavyo. Tayari nimeongea na mheshimiwa wetu na ameahidi kutusaidia,” akasema Okenye.
Swala hilo lilichipuka wiki moja iliyopita baada ya wazazi walio na watoto shule hiyo kutishia kuandamana wakitaka mwakilishi huyo kuwasaidia.
Samson Onchieku, mzazi katika shule hiyo, alisema kuwa vyoo hivyo ni hatari kwa afya ya wanafunzi na waalimu.
onchieku amependekeza hatua ya haraka kuchukuliwa ili kujenga zingine kabla ya watoto kufungua shule.
“Namwomba mwakilishi wetu Okenye kujenga vyoo haraka sana ili wanafunzi wakirudi wapate ujenzi umekamilika,” akasema Onchieku.