Wazazi wa vijana 17 waliokamatwa katika msako mjini Mombasa kwa madai ya kuhusika na visa vya uhalifu wamejitokeza na kudai kwamba watoto wao walinyimwa haki zao za kimsingi walipokatwa.
Wazazi hao wamesema kuwa askari waliwapiga vijana hao na kuwajeruhi jambo walilosema kwamba ni kinyume cha sheria.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Mombasa, wazazi hao walisema kuwa wanataka haki itendeke licha ya watoto wao kuwa washukiwa wa uhalifu.
“Hatujapinga shughuli za mahakama lakini tunapinga vile askari walivyowawatesa watoto wetu. Kwanini mtoto mdogo anapigwa mpaka anajeruhiwa kiasi hicho,” alisema Zaituni Swairina, mmoja wa wazazi hao.
Wazazi hao pia walidai kuwa hawakuruhusiwa kuwaona watoto wao walipozuru mahakamani, huku waikdai kuwa tangu walipofikishwa huko, wamekuwa wakinyimwa chakula.
“Mimi nilienda kumpelekea mwanangu chakula lakini hata nikimpa anashindwa kushika kwa sababu mkono ulikuwa umeumia sana,” alisema Fatuma Mohamed.
Vijana hao wenye umri wa miaka kati ya 12-26 walikamatwa usiku wa kuamkia siku ya Jumapili katika maeneo ya Buxton katika msako ulioendeshwa na maafisa wa polisi.
Polisi walisema kuwa vijana hao walipatikana na silaha kama vile panga na kudai kwamba wamekuwa wakiwahangaisha wakaazi wakati wa usiku.