Wazazi walio na watoto wanaoishi na ulemavu wamehimizwa kuwatembelea watoto wao katika shule wanazosomea ili kuwapa motisha.
Kwenye mahojiano na mwanahabari huyu mjini Mombasa siku ya Ijumaa, mwalimu wa shule ya Portreizt, Kaunti ya Mombasa, Saumu Athman, alisema hatua hiyo itawapa moyo watoto hao, na kuwafanya kujihisi wako sawa na watoto wengine katika jamii.
Athman alisema ni jambo la kusikitisha kuwaona wazazi wengi wakikosa kuwatembelea watoto wao shuleni.
“Tunashangazwa na jinsi baadhi ya wazazi wa watoto hao wanavyowajibikia majukumu yao. Wengi wa wazazi huwa hawawatembelei wanao na inaonekana kama wamewatenga. Hatua hiyo sio nzuri kwa vile lazima wazazi wawatambue wanao,” alisema Athman.
Mwalimu huyo ameongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja katika jamii kuhakikisha kuwa wanawapa moyo walemavu kwa kuwaleta karibu nao na kuwahusisha katika shuguli mbali mbali za maendeleo.