Wazazi katika shule ya msingi ya Amabiria eneo bunge la Nyaribari Masaba kaunti ya Kisii wamefunga shule hiyo rasmi kwa kile walichokisema ni utepetevu na uongozi mbaya wa mwalimu mkuu.
Kulingana na wazazi hao mwalimu mkuu wa shule hiyo Alice Osierio ana uongozi mbaya uliopelekea shule hiyo kutofanya vyema katika mtihani wa kitaifa wa darasa la nane mwaka jana ndiposa wakaamua kufunga shule hiyo ili mwalimu huyo ahamishwe kwengine.
Akizungumza katika eneo la Keumbu chifu wa Lokesheni hiyo Jonathan Machoka alisema wazazi hao walienda moja kwa moja hadi afisi za elimu katika eneo hilo na kutaka mwalimu huyo ahamishwe kwingine baada ya kufunga shule hiyo.
“Hii shule imefungwa na wazazi ambao wanahitaji mwalimu mkuu ahamishwe kufuatia matokeo duni ya mtihani na hili ni jambo ambalo si la kufurahisha kwani kuna sheria ambazo zinastahili kufuatwa,” alisema Machoka.
Aidha, mwalimu huyo mkuu naye alisema naibu wake ndiye anatumika na wazazi ili kumuondowa na kuchukua nafasi yake ya kuwa mkuu wa shule hiyo jambo ambalo limeleta utata mkubwa.