Mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Chache kaunti ya Kisii Richard Tong'i amewahimiza wazazi kushirikiana na walimu kuinua viwango vya elimu katika shule zote za kaunti hiyo.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa wazazi hawashirikiani na walimu jambo ambalo hupelekea uwepo wa matokeo duni katika mitihani ya kitaifa.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika shule ya upili ya Nyaguta iliyoko eneo bunge lake la Nyaribari chache, Tongi aliwaomba wazazi na walimu kushirikiana na kufanya kazi pamoja.
“Naomba kila mzazi kuwa awe katika mstari wa mbele kuunga mkono elimu kwa kushirikaiana na walimu ili shule za Kisii zifanye vyema katika mtihani,” alisema Tong’i.
“Kwa mzazi uridhi ambao utamwachia mtoto ni elimu wala sio chochote nahimiza kila mzazi awajibike kwa kusomesha mtoto wake kikamilifu,” aliongeza Tong’i.
Wakati huo huo, mbunge huyo aliomba wanafunzi nao kutia bidii katika masomo kwani huwa vigumu kwa wasio na elimu kusaka kazi katika serikali ya kitaifa na zile za kaunti.
Aidha aliomba walimu nao kuwa na motisha wanapowasomesha wanafunzi.
Mbunge Tongi pia aliwaomba viongozi wote wa kaunti hiyo ya Kisii kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kuwa shule za Kisii zinafanya vyema katika mtihani.