Kiranja wa Shirika la Nyanza Initiative for Girls Education and Empowerment (NIGEE) Profesa Kawango Agot, ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wa kike wanapata elimu sambamba na wale wa kiume.

Share news tips with us here at Hivisasa

Agot alisema kuwa shirika hilo, linaendelea kuweka mikakati ya kuona kuwa idadi kubwa ya wasichana katika kaunti za Kisumu, Migori, Siaya na Homabay wanasoma, akisema kuwa kumuelimisha mtoto mmoja wa kike ni sawa na kuelimisha jamii nzima.

“Shirika la Nigee lilianzishwa mwaka 2011, na kufikia sasa tunajivunia kuwarejesha wasichana 300 shuleni,” alisema Agot.

Naye mkewe gavana wa Kisumu Jack Ranguma Bi Olivia Ranguma, alisema kuwa wasichana wengi huacha masomo kutokana na ndoa za mapema, mimba za mapema na kukosa karo.

Hata hivyo, aliongezea kuwa visa vya watoto wasichana kuacha shule vimepungua maradufu katika kaunti ya Kisumu.

Kwa upande wake, waziri wa elimu kwa vijana na michezo katika serikali ya kaunti ya Kisumu Jenipher Kere, alisema kuwa serikala ya kaunti inabuni kanuni zitakazo hakikisha kuwa watoto wa kike katika kaunti ya Kisumu wanapata elimu.

Watatu hao walisema hayo kwenye uwanja wa Jomo Kenyatta jijini Kisumu mwishoni mwa juma, wakati wa Harambee iliyoandaliwa na Shirika hilo la Nigee, kuchangisha pesa za kuwalipia karo wasichana zaidi ya 300.

Jumla ya zaidi ya shilingi laki tano zilichangishwa katika hafla hiyo.