Wazazi kutoka ukanda wa Pwani wamehimizwa kufuatilia mienendo ya wanao ili kuhakikisha kuwa wanafahamu vyema maswala ya dini.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Hatua hiyo inanuia kuhakikisha kuwa vijana hawapotoshwi na kujiunga na itikadi kali.

Mwanaharakati wa akina Mama katika kundi la ‘Mothers Initiative Amani Kenya’ Mariam Wambui, amesema kuwa iwapo wazazi watafuatilia mienendo ya wanao na kuwaaelekeza vyema, basi maswala ya itikadi kali yatadhibitiwa.

Akizungumza katika kikao cha kuwahamasisha wanawake na vijana kuhusu maswala ya itikadi kali mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Wambui alisema kwamba ni sharti wazazi wawe karibu na watoto wao, ili kuona kwamba hawapotoshwi kimaadili wala kidini.

Wambui alisema kuwa kutokana na hamasa za kina ambazo zimekuwa zikiendelezwa katika jamii tangu mwanzoni mwa mwaka huu, kumekuwepo na mabadiliko makubwa hasa miongoni mwa vijana.

“Tunawaomba wazazi kufatilia mienendo ya watoto wao ili kuwakinga na makundi ya kigaidi. Japo tunaendeleza hamasa mashinani, kuna umuhimu wa swala hilo kuangaziwa,” alisema Mariam.

Kulingana na kundi hilo la akina mama, kufikia sasa idadi ya vijana ambao wamekuwa wakisajiliwa kujiunga na makundi ya kigaidi imepungua kwa kiwango kikubwa.