Mwenyekiti wa Kamati ya bunge la kaunti ya Mombasa kuhusu Vijana, Michezo na Jinsia Serah Nyamvullah amewataka wazazi kujitokeza na kuwashauri vijana kubuni miradi mbalimbali ya kimendeleo ili kufaidika na fedha kutoka serikali za kaunti.
Akiwahutubia wakazi wa mjini Mombasa siku ya Jumanne, Nyamvullah, ambaye pia ni mwakilishi maalum katika bunge hilo amesema kuwa iwapo vijana watachukua fursa hiyo, basi watafaidika na kuwawezesha kujitenga na maswala ya kihalifu na mihadarati.
Kulingana na Nyamvullah, vijana wengi katika kaunti ya Mombasa wamejitosa katika uhalifu na utumizi wa mihadarati kutokana na kukosa hamasisho la kutambua mbinu mbalimbali za kuwawezesha kujikimu kimaisha, na akawahimiza wazazi kuwashauri vijana wao kutembelea afisi za Wizara ya Vijana, Michezo na Jinsia kusaidiwa kupata zabuni.
"Tafadhalini ndugu zangu, vijana wetu hawa iwapo hatutawasaidia na kuwashuri, basi usalama hatutauimarisha, lazima wajihusishe na mambo ya kubuni ajira na kujiunga na makundi ili kufaidika na mipango ya serikali ya kaunti ya kuwasaidia vijana," alisema Nyamvullah.
Wakati huo huo, amewahimiza wanawake kuhakikisha kuwa wanabuni makundi ya akina mama ili kufaidika na miradi kutoka kwa serikali kuu na kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa wanajihusisha na maswala ya kimaendeleo ili kujikimu vyema kimaisha.
Kiongozi huyo amewahimiza vijana kujitenga na baadhi ya watu wanalenga kuwapotosha kimaadili na kuhakikisha kuwa wanatekeleza maswala muhimu ya kuimarisha uchumi wa kaunti hiyo kwa kujihusisha na ubunifu wa ajira.
Picha: Wakazi wa kaunti ya Mombasa wakikongamana katika mkutano wa hamasisho. Wamehimizwa kuwashauri vijana wao kujitenga na uhalifu na utumizi wa mihadarati ili kujihusisha na maswala ya kimaendeleo. HokaM/Hivisasa.com