Wazazi Mombasa wameelezea shaka yao watoto kujihusisha na utumizi wa madawa ya kulevya kwa sababu ya mgomo wa walimu unaondelea.
Pia, wamesema kuwa wanao huenda wakashawishika kujiunga na makundi haramu ya kigaidi.
Wazazi hao wametoa hofu yao kwa kusema kuwa sasa watoto wengi wako nyumbani na hawana la kufanya. Wazazi hawa wanasema juu ya ukosefu wa walimu, huenda vijana walio na mawazo mabaya ya kigaidi kuwapotosha. Wameitaka serikali kutafuta mbinu mwafaka ya kusuluhisha suala la mishahara ya walimu.
Wakiongozwa na Fatma Hassan, wazazi hao walisema kuwa kwa sasa wazazi wengi wana kazi zao na biashara hujihusisha nazo na huwaacha watoto wao nyumbani na kinachoendelea wakati hawamo hawajui. Waliongeza kuwa ni rahisi kwa watoto hao kuanza kutumia dawa za kulevya na hata kuingilia mambo ya ugaidi.
“Hii itakuwa nafasi ya watoto wetu kujipata pabaya hasa katika jiji hili letu la Mombasa ambalo lina aina zote ya uhalifu. serikali kama kweli inataka kupigana na masuala ya ugaidi na matumizi ya dawa za kulevya, sharti watoe mwongozo sasa hivi na kwa dharura,” alisema mzazi huyo.
Kwa upande wake Joyce Aketch ambaye hupigania haki za watoto dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya katika kaunti hiyo, serikali inapoendelea kufanya siasa kuhusiana na suala la mgomo wa walimu, wanaoathirika zaidi ni watoto.