Wanawake watatu wametiwa mbaroni baada ya kuhusika katika kuwakeketa watoto wao wasichana wanne wa kati ya umri wa miaka tano hadi tisa kijiji cha Nyaisa wilayani Manga kaunti ya Nyamira.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na naibu wa chifu katika kata ya Morako, Jeremiah Ogendi, walipata fununu kutoka kwa wanakijiji na walipofika kwenye boma hiyo waliwavumania watatu hao wakiwemo wazazi wawili wa watoto hao na nyanya yao huku mwanamke mmoja aliyekuwa akitekeleza uovu huo akifanikiwa kutoroka.

"Tulipofika kwenye boma hiyo tukiandamana na maafisa wa polisi tulipata kuwa tayari wasichana hao wamekeketwa na tukawatia mbaroni wazazi wao na nyanya lakini mshukiwa mmoja akafanikiwa kutoroka," alisema Ogendi.

Ogendi amesema kuwa watoto hao walipelekwa hospitalini na kutibiwa na wako salama wakati maafisa wa polisi wanamsaka mkeketaji huyo anayesemekana kutoka wilaya ya Kisii ya kati katika kaunti ya Kisii.

"Daktari amethibitisha kuwa watoto hao walikeketwa na wametibiwa na kukubaliwa kurudi nyumbani akiongezea kuwa hali yao iko salama," aliongezea Ogendi.