Mwandishi wa vitabu vya fasihi ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Catholic University of East Africa Profesa Clara Momanyi amelaumu wazazi na jamii kwa jumla kwa visa vya kuchomwa kwa shule.
Momanyi amesema maadili ya wanafunzi hao yanaanzia nyumbani kabla kufika shuleni.
Katika mahojiano ya moja kwa moja na mwandishi huyu kwenye kongamano la kitamaduni mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Momanyi alishauri wazazi kutowalaumu walimu kwani wao ndio walioshindwa kuwakuza watoto wao vyema.
“Huwezi kulaumu mwalimu kwa sababu mwalimu anampokea mtoto kutoka kwa mzazi akiwa tayari amelelewa katika ule utamaduni wake. Wazazi wana jukumu kubwa sana ambalo walilitupia mkono kitambo,” alisema Momanyi.
Profesa huyo alimtaja mama kama mtu muhimu katika kulea na kukuza maadili ya mtoto nyumbani tofauti na baba.
Hata hivyo, aliongeza kwamba maisha sasa yamebadilika kwani wazazi wengi wa kike wanajishugulisha na mambo mengi ya nyumbani na kusahau watoto wao tofauti na hapo zamani.
Nilipomuliza iwapo anakubaliana na wale wanaopendekeza adhabu ya kiboko shuleni ili kuzuia matukio kama hayo ya shule kuchomwa, Profesa Momanyi alisema kuwa hapo zamani kiboko kilitumika vyema shuleni lakini baadhi ya walimu siku hizi wanakitumia visivyo.
“Ukiangalia katika mukhtadha na jinsi kiboko kilitumika kitambo kilikuwa na mipaka yake. Shida ni kwamba je, mwalimu wa leo atakitumia na mipaka ama atakitumia kummaliza mwanafunzi?” aliuliza Momanyi.
Wakati huo huo, msomi huyo aliishauri serikali kuweka kikao cha pamoja na wadau wote katika sekta ya elimu bila kuwasahahu wazazi, walimu na wanafunzi ili kutafuta suluhu la tatizo hilo.
Kauli yake inajiri huku zaidi ya shule 100 zikiathiriwa na mikasa ya moto.