Katibu mkuu wa muungano wa wazazi nchini Musau Ndunda amemlaumu Waziri wa Elimu Fred Matiang’i kufuatia misururu ya migomo inayoshuhudiwa katika shule nyingi nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano ya simu na mwandishi huyu siku ya Jumanne, Ndunda alidai kuwa hatua ya Matiang'i kutowahusisha wadau wote wa elimu wakiwemo wazazi katika kutatua shida zinazokumba baadhi ya shule ni miongoni mwa sababu zinazochangia migomo hiyo.

“Matiang’i amechukua suala la elimu kama biashara yake ya kibinafsi. Sisi wazazi tunatengwa kila mara kunapotokea jambo shuleni. Anakaa chini na hao walimu wakuu wanazungumza kivyao lakini mambo yakizidi ndipo tunatafutwa,” alisema Ndunda.

Aidha, Ndunda alidai kuwa baadhi ya walimu ambao hawana uhusiano mwema na usimamizi wa shule huenda wanashirikiana na wanafunzi kutekeleza uharibifu shuleni, kama njia mojawapo ya kuonyesha ghadhabu zao.

Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi hushiriki migomo kama njia moja ya kulipiza kisasi hasa baada ya kuadhibiwa na usimamizi wa shule kutokana na makosa waliofanya.

“Wakati mwingine wanafunzi waliotimuliwa shuleni baada ya kukosea hupanga njama kisha wanachoma shule ili kuwazuia wenzao kuendelea na masomo,” alisema Ndunda.

Waziri Matiang'i kupitia barua iliyotumwa kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne, alitaja mbinu mbovu za uteuzi wa wanafunzi, wizi wa mtihiani, matumizi ya dawa za kulevya na siasa duni kama vyanzo cha migomo hiyo.

Aidha, Matiang'i alilaumu usimamizi duni kutoka kwa wakuu wa elimu na wadau wengine katika sekta hiyo kwa baadhi ya mambo yanayosababisha wanafunzi kutetekeza shule.

Haya yanajiri baada ya zaidi ya shule 68 kuathirika kutokana na mikasa ya moto inayoendelea kushuhudiwa katika shule mbali mbali nchini.