Kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Laban Masira amejitokeza kuwarahi wakazi wa kaunti hiyo hasa kwenye eneo lake la uwakilishi kukumbatia chanjo dhidi ya ugonjwa wa surua miongoni mwa watoto. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu, Masira alisema kuwa yafaa wazazi waandamane na watoto wao hadi kwenye vituo vya afya mahala ambapo chanjo hiyo itakuwa ikipeanwa. 

"Ni ombi langu kwa wazazi katika kaunti hii hasa kwenye eneo la wadi ya Nyamaiya kukumbatia kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa surua kwa kutembelea vituo maalum vya afya vilivyotengwa wakiwa na wanao ili waweze kupata chanjo hiyo," alisema Masira. 

Masira aidha aliongeza kwa kuwasihi wakazi wa eneo lake la wadi hasa kwenye timbo la uchimbaji mawe la Rangenyo kutahadhari. 

"Huu ni msimu wa mvua na kawaida kunashuhudiwa hatari hasa kwenye timbo za mawe, na ndio maana nawarahi wakazi wa eneo la Rangenyo kutahadhari kuchimba na kupasua mawe msimu huu," aliongezea Masira.