Naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Likoni Geoffrey Omoding amewaomba wazazi katika eneo hilo kushirikiana na maafisa wa usalama katika vita dhidi ya uhalifu.
Akizungumza na wanahabari siku ya Alhamisi katika afisi yake, Omoding alisema kuwa wakati wa wazazi kuanza kujukumika umefika.
“Ni jambo la kusikitisha kuona vijana wenye umri mdogo wakijihusisha na visa hatari vya uhalifu. Ningependa kuwaomba wazazi kushirikiana na idara ya usalama ili vijana hao waweze kurejeshwa katika njia iliyo sawa,” alisema Omoding.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya vijana wanane wanaoaminika kuwa wanachama wa kundi ambalo limekuwa likiwahangaisha wenyeji kujisalimisha kwa polisi.
Idadi ya vijana waliojisalimisha kwa polisi imeongezeka hadi 27 baada ya wengine 19 kufika mbele ya kituo cha polisi katika eneo hilo na kukiri kuhusika na uhalifu.
Vijana waliojisalimisha kwa idara ya usalama wiki hii walikuwa wa kati ya umri wa miaka 11 na 18.