Huku wanafunzi wakielekea nyumbani kwa likizo ya muhula wa kwanza kote nchini, walimu kutoka shule ya msingi ya Amani wamewataka wazazi kuwa waangalifu zaidi na wanao watakapokuwa nyumbani kwa muda wa takribani mwezi mmoja.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Onesmus Mtie wazazi wanapaswa kuwa waangalifu zaidi wakati huu ambapo kwa sasa kumekuwepo na visa vingi vya watoto wa shule kupachikwa ujauzito.

Aidha mwalimu huyo pia amewasihi wazazi kuchukua jukumu la kuchunguza mienendo na safari ambazo wanawao hupenda kuzibuni wakati wakiwa kwenye likizo akisema kuwa pia hizo huchangia pakubwa katika kuharibika kwao wakiwa likizo.

Kwa upande wake naibu mwalimu mkuu wa shule ya St Mary’s katika eneo la Bangla amewataka wazazi kuhakikisha kuwa watoto wanadurusu vitabu vyao wala sio kuwaachilia kucheza kila wakati kwa kisingizio kuwa ni wakati wa likizo. 

Mwalimu huyo aidha ametoa wito kwa wazazi kutowaruhusu wanawao kuhudhuria sherehe wasizokuwa na fahamu nazo kwani huwashawishi wanafunzi kushiriki vitendo viovu.

Walimu hawa aidha wameonekana kuzungumzia zaidi kuhusiana na ongezeko la visa vya watoto wanafunzi kupata mimba za mapema nyakati za likizo huku wakisema kuwa kwa sasa kaunti ya Mombasa na eneo zima la Pwani kwa ujumla linapaswa kuangazia zaidi usalama wa wananfunzi wanapokuwa kwenye likizo kwani hivi majuzi kaunti ya kwale ilitajwa kuongoza katika visa vya watoto wanafunzi waliona ujauzito katika eneo la Pwani.

Hata hivyo wamesema kuwa kufikia sasa kaunti zote zinastahili kuweka mikakati ya kukabiliana na swala hilo ambalo wamelitaja kama janga miongoni mwa wanafunzi.