Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Nakuru Thomas Sankei, amewaonya wazazi na walezi dhidi ya matumizi mabaya ya pesa msimu huu wa sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.

Sankei alisema kuwa wazazi wanapaswa kukumbuka kuwa shule zitafunguliwa mwaka ujao.

Akizungumza afisini mwake siku ya Alhamisi, Sankei aliwashauri wazazi kutumia kile walichonacho kwa njia nzuri, badala ya kutumia pesa nyingi ili kuwafurahisha wapendwa wao msimu huu wa sherehe, na kisha kujuta baadaye.

“Wazazi wanapaswa kuyapa kipaumbele maswala na mahitaji yenye umuhimu mkubwa katika familia zao, badala ya kutumia pesa ambazo zingetumika katika kulipia karo za shule , kodi ya nyumba na mahitaji mengine,” alisema Sankei.

Sankei aidha aliwashauri waliyokwenye ndoa kuwa na mawasiliano mema kila mara katika kufanya uamuzi msimu huu la si hivyo huenda ndoa nyingi zikavunjika na kusambaratika katika kipindi hiki cha sherehe.

Aliwatakia wakaazi wa Kaunti ya Nakuru Krisimasi njema na mwaka mpya wa 2016 wenye mafanikio.

Aidha, alitoa wito wa wakaazi kuwakumbuka wale ambao hawajiwezi katika jamii, kwa kushirikiana nao kwa hali na mali.