Wazazi katika kaunti ya Nakuru wametakiwa kujitolea ili kuimarisha viwango vya shule za umma, kwa kujitolea kuchangia katika ujenzi wa shule na ununuzi wa vifaa vya kisasa.
Akiongea siku ya Ijumaa katika shule ya msingi ya Kiamaina katika wadi ya Bahati wakati wa mchango wa kununua basi la shule, afisa mkuu wa elimu katika kaunti Catherine Kitetu, aliwahimiza wazazi kukoma kuitegemea serikali kuwajengea shule.
Alisema kuwa wazazi wana jukumu kubwa sana katika kuimarisha viwango vya shule ambazo watoto wao wanasomea.
“Zamani wazazi walikuwa wanashirikiana katika kujenga mashule na kununua vifaa vya shule lakini tangu elimu bila malipo ianze wazazi wengi wamedhani kwamba jukumu hilo ni la serikali pekee na hii imepelekea kudorora kwa viwango vya elimu katika shule nyingi za umma,” alisema Kitetu.
“Iwapo mnataka watoto wenu wasome vyema na katika mazingira bora, basi itabidi nyinyi kama wazazi mchangie katika kuimarisha na kuboresha mazingira ya elimu katika shule zetu na tuwache kuitegeea serikali,” aliongeza kusema.
Kitetu aliwataka wazazi katika shule za umma kuchukua mfano kutoka kwa wenzao katika shule za kibnafsi ambao wanachangia pakubwa katika kuimarisha viwango vya shule zao.
Alisema kuwa serikali ya jimbo imejitolea kuhakikisha kuwa shule zote za umma katika jimbo zinapata vifaa vya kisasa vya masomo ili kuinua viwango vya masomo katika jimbo.
“Serikali yetu imejitolea kuona kwamba shule zetu zinafikia viwango vinavyotakikina kimataifa ilituweze kuwapa watoto wetu mazingira mazuri ya kusomea,” alisema Kitetu.