Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mariwa iliyoko Kata ya Ahero Andrew Aguka amewataka wazazi kukomesha biashara ya pombe miongoni mwa wanafunzi na badala yake kuwajibikia elimu ya wanao kikamilifu.
Akizungumza kwenye mkutano na wazazi katika shule hiyo mnamo siku ya Jumanne, mwalimu Aguka alisema kuwa watoto katika shule hiyo hawafanyi vyema kwenye mtihani huku wengine wakiacha masomo kighafla baada ya kuchelewa kuwa shuleni kila mara.
“Kama mwanafunzi atashiriki biashara ya pombe basi tusidanganyike kwamba tunatarajia kizazi bora kwenye siku zijazo. Mmeachia wanafunzi majukumu ya familia zenu huku mkiwa mmewatwika mzigo wa kujitafutia karo ya masomo yao wenyewe,” alisema mwalimu Aguka.
Duru za kwaminika zilisema kwamba baadhi ya wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo wameingilia ulevi kupita kiasi na karibu kila boma vijijini hutegemea biashara ya pombe kukimu maisha yao.
Akijadili swala hilo, mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Jared Omollo alihoji kwamba baada ya biashara hiyo kushamiri miongoni mwa jamii za eneo hilo, wazazi wengi wanawashirikisha wanao ambao wangali shuleni kugema pombe wakiwaagiza kuwa sehemu ya fedha zinazotokana na bidii yao kwenye kazi hiyo ndizo watakazolipiwa karo.
Calistus Oyoo ambaye ni mmoja wa wazazi wa shule hiyo alishtumu vikali tabia hiyo akisema kuwa ndiyo imechangia wanafunzi wengi kuacha shule, ikizingatiwa kuwa baadhi yao huanza kunywa pombe na kushiriki anasa.