Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku asilimia kubwa ya shule zikiwa zimefunga kwa likizo ya Disemba, wazazi wametakiwa kuwa makini na kuwachunga wanao ili kuwaepusha dhidi ya kujiunga na makundi ya uhalifu.

Hiyo ni mbinu moja ya kuwaweka vijana karibu na jamii ikizingatiwa kuwa nyakati za likizo, watoto wengi ambao wako nje wana huru wa kutembea na kukutana na marafiki wao wengine huenda wakawa na ushawishi ambao si mzuri kwao.

Haya yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Elimu katika Kaunti ya Mombasa Abdikadir Kike, ambaye alisisitiza umuhimu wa wazazi kuwaongoza wanao, wakati huu wa likizo ndefu ya Disemba na kuwashauri kuwaangalia kwa karibu.

Bw Kike ambaye aliongea na mwandishi wa habari huyu kwenye ofisi yake siku ya Ijumaa, aliweka wazi baadhi ya hatari ambazo zinawakodolea macho watoto kama utumizi ya dawa za kulevya, mafunzo ya itikadi kali na ushawishi wa kujiunga na makundi ya uhalifu na yale ya kigaidi.

Aidha, mkurugenzi huyo aliwataka wazazi kuhakikisha kuwa watoto wanahusishwa kwenye shughuli mbambali kama vile kusoma vitabu vya dini hasa wale walio Waislamu wahakikishe kuwa wanaenda katika Madrasa, na wale wa Kikristo kuenda kanisani kama njia moja ya kujiweka karibu na Mungu.