Kamati ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa ukimwi eneo bunge la Changamwe imewataka wazazi na viongozi wa kidini kuwa katika mstari wa mbele kuwaelekeza vijana katika maadili mema.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Maurice Ochieng, amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la maambukizi ya maradhi ya ukimwi miongoni mwa vijana.
Bwana Ochieng alisema kuwa vijana wengi wa umri kati ya miaka 11 na 35 katika eneo la Changamwe wameathirika na ugonjwa huo, kutokana na kushiriki tendo la ndoa bila kutumia kinga.
Kamati hiyo pia imesema kuwa japo ni jukumu la wazazi kuzungumzia swala la ugonjwa huo, wazazi wa eneo hilo wamezembea na hata kuogopa kuzungumzia ugonjwa huo kwa kisingizio kuwa maswala hayo hayaambatani na kanuni za mila na desturi zao.
“Ikiwa wazazi wanahofia kuwafundisha wanao maadili mema kwa kutoa mifano ya magonjwa kama hayo na namna yanavyosambazwa, basi itakuwa vigumu kwa jamii nzima katika eneo la Pwani kulishughulikia swala hilo,” alisema Ochieng.
Ochieng amewaomba viongozi wa kidini kuandaa kongamano katika eneo hilo ili kuwahamasisha vijana kuhusu athari za magonjwa ya zinaa.