Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amewataka wazazi kuwapa watoto wao malezi bora na kuwaonya dhidi ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi.
Akizungumza siku ya Jumapili katika bustani ya Treasury Square jijini Mombasa, Nassir aliwasihi wazazi kuwa mstari wa mbele kukomesha visa vya ugaidi na uhalifu katika ukanda wa Pwani.
Aidha, aliongeza kuwa itakuwa bora iwapo vijana hao watahusishwa na makundi ya kujiendeleza badala ya kuingilia makundi ya ugaidi.
“Wahusisheni vijana wenu katika makundi ya maendeleo ili visa vya ugaidi vipungue katika eneo hili,” alisema Nassir.
Aidha, amewataka wazazi kutowalaumu maafisa wa polisi pindi wanapoitekeleza kazi yao ya kuwakamata vijana wahalifu.
Kauli yake inajiri kutokana na kuendelea kushuhudiwa vijana wengi wakijiunga na makundi ya kigaidi.