Mwenyekiti wa muungano wa wazazi eneo la Nyanza, Jackson Omollo, ameunga mkono hatua ya serikali kufutilia mbali mfumo wa kuorodhesha shule na wanafunzi kulingana na matokeo ya mitihani ya kitaifa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katika kikao na wanahabari mjini Kisumu siku ya Jumanne, Omollo alisema kuwa kuorodheshwa kwa shule na wanafunzi kunahujumu baadhi ya shule nchini, hasa zile zilizo na miundo msingi duni.

Mwenyekiti huyo alisema hatua hiyo itawapa wanafunzi motsiha ya masomo, hasa wale wanaokabiliwa na changamoto za ukosefu wa vifaa muhimu vya elimu.

 “Sisi kama wazazi wa Nyanza, tumekaribisha hii maneno ya kufutiliwa mbali kwa mfumo wa kuorodhesha shule kulingana na matokeo ya mithani ya darasa la nane KCPE na kidato cha nne KCSE. Hatua hiyo italeta usawa katikasekta ya elimu nchini,” Omollo alisema.

Siku ya Jumatatu, Maafisa wa chama cha walimu nchini (Knut), walipinga hatua ya Wizara ya Elimu kufutilia mbali mfumo wa kuorodhesha shule na wanafunzi kulingana na matokeo ya mitihani ya kitaifa.

Katibu mkuu wa muungano huo Wilson Sosion alisema wizara ya elimu ilifaa kushauriana na wadau wote kabla ya kutoa agizo hilo.

Juma lililopita, Wizara ya Elimu ilitoa agizo hilo kwa lengo la kumaliza visa vya udanganyifu wakati wa mitihani ya kitaifa.

Sossion alidai kuwa kuondolewa kwa mfumo wa kuorodhesha shule na wanafunzi nchini, kunatishia kuiweka Kenya miongoni mwa nchi zilizofeli katika sekta ya elimu.