Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi kutoka kaunti ya Nyamira wamelaumu  usimamizi wa chuo kikuu cha Kisii kwa kufungua matawi mengi ya chuo hicho bila kuzingatia masharti muhimu na kusababisha kufungwa kwa baadhi ya matawi ya chuo hicho.

Kulingana na wazazi hao, ni hasara kwao kwani wengi wao tayari wamelipa karo ya muhula wa kwanza na kuomba usimamizi huo kuwajibika na kutafuta njia ya kuwasaidia mapema.

Wakizungumza siku ya Jumanne mjini Nyamira,  wazazi hao wakiongozwa na Victor Masanya na Geoffrey Orina walikosoa na kulaumu usimamizi wa chuo hicho kwa kutofuatilia masharti muhimu wanapofungua matawi ya chuo hicho.

“Wengi wetu tulikuwa tayari tumelipa karo ya shule sasa tutafanya nini na tumechoshwa na chuo hiki maana badhi ya matawi hapa Nyamira yamefungwa,”  Victor Masanya alisema.

“Tunaomba usimamizi wa chuo hicho kuharakisha kupanga jinsi watoto wetu wataendelea na masomo kabla ya miezi hiyo walipewa mitatu ili kuwajibika,”  Geoffrey Orina alisema.

Mnamo siku ya Jumanne msimamizi wa elimu ya vyuo vikuu nchini David Some alifunga matawi 10 kati ya matawi 13 ya chuo cha Kisii.