Zaidi ya wazee 300 wa Kaya wa jamii ya Wamijikenda kutoka kaunti tatu za Pwani walizuru Ikulu ya Rais mjini Mombasa siku ya Jumatano.
Ziara ya wazee hao kutoka kaunti ya Mombasa, Kilifi na Kwale ni kutokana na mwaliko waliokuwa wametuma kwa Rais Uhuru Kenyatta.
Wazee hao walijadili maswala ya maendeleo na kuangazia changamoto zinazowakumba Wapwani kwa ujumla.
Katibu mkuu wa Malindi District Association, Joseph Mwarandu, katika mahojiano alisema kwamba ziara hiyo sio ya kisiasa, huku akieleza matumaini kwamba mkutano huo utakuwa na manufaa kwa wakaazi wa Pwani.
“Huu sio mwaliko wa kisiasa, tulikuwa tumetuma maombi kwa rais na akasema kuwa atakutana nasi na leo tunashukuru kwamba ametualika rasmi,” alisema Mwarandu.
Kiongozi huyo wa Kaya amesema tangu Rais Kenyatta kuingia uongozini, amekuwa akionyesha nia yake ya kuwahusisha vijana na wazee katika maswala mbalimbali ya jamii.
Aidha, alisema serikali zilizopita zimekuwa zikiwaacha wazee nyuma, huku akisisitiza kwamba wazee wana umuhimu mkubwa.
“Wazee tumekuwa tukionekana kwamba hatukusoma na hatujui lolote, lakini lazima serikali ihusishe wazee kwa sababu tunafahamu mambo mengi yanayoathiri taifa,” alisema Mwarandu.
Wazee hao walitaja baadhi ya miradi ambayo imesimama kwa muda mrefu kama vile kiwanda cha maziwa na kile cha korosha katika Kaunti ya Kilifi, huku wakiitaka serikali kuvifufua tena.
Aidha, aliongeza kwamba rais aliwaahidi kwamba atarudi tena Pwani ili kufanya kikao kingine ambapo watajadili maswala ya siasa na uongozi.