Wazee wa jamii ya Mijikenda katika ukanda wa Pwani wamepinga maandamano yanayofanywa na mrengo wa upinzani nchini Cord kushinikiza kubanduliwa kwa makamishna wa Tume huru ya mipaka na uchaguzi nchini IEBC.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongozwa na katibu wa muungano wa Malindi District Cultural Association (MADCA) Joseph Mwarandu, wazee hao walisema maandamano hayo yanahatarisha maisha ya wananchi pamoja na uharibifu wa mali.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa baraza la jamii ya Mijikenda nchini Vincent Mwachiro alisema kuwa maandamano hayo huenda yakaleta mgawanyiko miongoni mwa Wakenya iwapo hayatasitishwa.

“Ningependa kuwahimiza viongozi wa pande zote mbili kujadiliana kuhusu namna ya kuifanyia IEBC marekebisho ili kurejesha imani ya wananchi ambayo tayari imeshuka kuhusu utendakazi wa tume hiyo,” alisema Mwachiro.

Kauli ya wazee hao inajiri huku mrengo wa Cord ikishikilia kuwa itaendelea na maandamano hayo kushinikiza Tume ya IEBC kubanduliwa, kwa madai kuwa tume hiyo haiwezi aminiwa kuusimami uchaguzi mkuu wa 2017.

Hata hivyo, Rais Uhuru Kenyatta akizungumza siku ya Alhamisi akiwa katika ziara mjini Mandera, aliseme kuwa sharti viongozi wa Cord wafuate sheria katika shinikizo zao za kutaka tume hiyo ifanyiwe maguezi.