Kamati ya usalama eneo bunge la Likoni imesema itaandaa mahojiano baina ya wazee wa mitaa katika eneo hilo ili kubaini wale wanaostahili kuachishwa jukumu la kusimamia mitaa.
Akizungumza siku ya Ijumaa huko Likoni, mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni naibu kaunti kamishna wa Likoni Geoffrey Omondi, alisema hiyo ni mojawapo ya mbinu za kupunguza visa vya baadhi ya wazee wa mitaa kupatikana wakishirikiana na magenge ya uhalifu katika eneo hilo.
Omondi alisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona kuwa visa vya utovu wa usalama vinazidi kuongezeka katika eneo la Likoni ilihali katika maeneo mengine visa hivyo vinadhibitiwa.
“Tufanya kila juhudi kuhakikisha kuwa mkaazi wa Likoni anaishi bila uoga wowote. Kumekuwa na ongezeko la magenge ya wezi yanayoaminika kushirikiana na wazee wa mitaa kutekeleza maovu,” alisema Omondi.
Aliongeza; “Wazee hao hupewa kiasi fulani cha pesa na vijana hao ili wawastiri endapo watapatikana wakitekeleza maovu. Ikiwa maafisa wa polisi wanaweza kuwakamata wahalifu bila ya wazee wa mitaa kujua basi ni ishara tosha kuwa kuna njama fiche baina ya wazee hao na magenge yanayotekeleza uovu eneo hili.”
Hata hivyo, alisema kuwa hali ya usalama Likoni imeimarishwa kufuatia taarifa za kijasusi kuwa magenge ya uhalifu yanaishi eneo hilo.