Wazee wa mtaa wanaohudumu katika mitaa mbalimbali mjini Mombasa wamependekeza serikali kuwatengea kiasi kidogo cha mshahara kama wafanyakazi wengine wa umma.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu nyumbani kwake, mama wa mtaa wa eneo la Barsheba ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa alisema kuwa wanapitia changamoto nyingi katika harakati za kuwahudumia wakaazi, hivyo itakuwa vyema iwapo serikali itawaangazia.

“Kazi tunayofanya sio rahisi. Tunahitaji angalau kupewa hata kama ni pesa kidogo ili nasi tujihisi kuwa kweli kuna mtu anatambua ile juhudi za kulinda na kuleta uwiano baina ya wakaazi,” alisema mama huyo wa mtaa.

Aidha, mama huyo alipinga madai ya baadhi ya wakaazi kuwa baadhi ya wazee wa mtaa wanahongwa ili kuegemea upande mmoja wakati wa kutatua kesi baina ya pande mbili zinazokinzana.

“Mimi tangu nianze kuhudumu kama mama wa mtaa sijawahi chukua hongo wala sipanii kula rushwa sababu hiyo ni kumnyima haki mtu anayehitaji haki itendeke,” aliongeza.

Kwa muda sasa, baadhi ya wakaazi mjini humo wamekuwa wakilalama kuwa baadhi ya wazee wa mtaa wanapokea hongo ili kupendelea upande mmoja, ama hata kutosikiliza malalamishi yanapowasilishwa kwao.

Aidha, wazee hao wa mtaa pia wamekuwa wakipitia changamoto za usalama huku wengine wao wakishambuliwa na vijana wanaodai wanawasaliti kwa maafisa wa usalama kuhusu maovu wanayotekeleza.