Waziri wa maswala ya afya kwenye serikali ya kaunti ya Nyamira Gladys Momanyi amejitokeza kusisitiza kuwa wizara yake imo mbioni kuimarisha huduma za afya katika kaunti hiyo.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu kutoka mjini Meru siku ya Alhamisi, Momanyi alisema kuwa wizara yake imetengewa shillingi billioni 1.2 kwenye mwaka wa kifedha wa 2015-2016, na anatumai pesa hizo zitafanikisha shughuli za utoaji huduma.
"Ni furaha kwamba bunge la kaunti ya Nyamira liliona vyema kuitengea wizara yangu pesa nyingi na hata kupiku wizara zingine, na kwa hakika nina imani kwamba shillingi billioni 1.2 zitatuwezesha kuwahudumia wagonjwa vyema," alisema Momanyi.
Momanyi aidha aliongeza kwa kusema kuwa tayari wizara yake imefanikiwa kuajiri zaidi ya wahudumu wa afya wapatao elfu 1,500, hali aliyosema itasaidia kaunti hiyo kukabiliana pakubwa na changamoto za ukosefu wa wahudumu wa afya wakutosha.
"Kumekuwa na changamoto za ukosefu wa wahudumu wa afya wakutosha kwenye hospitali zetu na ni furaha kwamba kupitia kwa bodi ya uajiri wa wafanyakazi PSB tumefanikiwa kuajiri zaidi ya wahudumu wa afya 1500 idadi ambayo itasaidia kupambana na ukosefu wa wahudumu wakutosha kwenye idara ya afya," aliongezea Momanyi.